Sheikh Riyadh Assenga (Abul Barakaat) حفظه الله ni miongoni mwa masheikh wanaojishughulisha na kufundisha na kueneza elimu ya dini kwa kufuata Qur-aan na Sunnah kwa uelewa wa Salafus-Swaalih. Ni katika masheikh wa Masjid na Markaz Omar bin Khattwab – Kariakoo, ambapo hushiriki kikamilifu katika utoaji wa darsa na malezi ya wanafunzi wa elimu ya dini. Amejikita katika kufundisha masomo mbalimbali ya Kiislamu, hususan ‘Aqiydah, Fiqh na masomo mengine, akitoa mafunzo yake kwa njia ya Darsa, Mihadhara, Semina na Khutba za Ijumaa.
Aidha, Sheikh Riyadh Assenga ni miongoni mwa masheikh waliopata elimu yao kutoka kwa wanazuoni wa Ahlus Sunnah katika nchi ya Saudi Arabia, jambo lililompa msingi imara katika uelewa wa dini na manhaj sahihi. Katika da‘wah yake, anajulikana kwa kusisitiza kushikamana na Tawheed na kujiweka mbali na Bida’a na aina zake zote, pamoja na kuhimiza kushikamana na manhaj ya Salafus-Swaalih. Ameendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha jamii, akilenga kueneza elimu yenye manufaa na kuimarisha uelewa sahihi wa Uislamu.